Рет қаралды 7,051
Serikali imejiridhisha na kasi ya ujenzi ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa unaojengwa Msalato jijini Dodoma, ambao utagharimu kiasi cha zaidi ya Sh300 bilioni hadi kukamilika kwake.
Hayo yamesemwa jana Mei 5, 2024 kwenye ziara ya Msemaji wa Serikali jijini Dodoma, ambayo ilikuwa na lengo la kukagua miradi ya kimkakati iliyoanzishwa na Serikali.
Akizungumza na wanahabari, Msemaji wa Serikali Mobhare Matinyi, ameonyesha kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa Uwanja huo, ambao kwa awamu ya kwanza utafanyiwa majaribio ya kutua na kuruka kwa ndege ifikapo mwezi Agosti mwaka huu.
Matinyi amesema kuwa matarajio ya Serikali baada ya uwanja huo kukamilika, ni kuwa utahudumia ndege za mashirika ya ndani na nje ya nchi.
“Si tu kuhudumia ndege hizo ila pia Dodoma itaongeza idadi kubwa ya watu ambao watachangia ongezeko la uchumi wetu, hivyo wananchi na wenyeji wa Dodoma waanze kujiandaa kuchangamkia fursa hii,” amesema Matinyi.