Рет қаралды 604
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umesikitishwa na vifo vya watu wawili ambao awali inadaiwa walikamatwa na maafisa wa mamlaka ya kuzuia na kupambana na dawa za kulevya kisiwani Pemba Zanzibar na kisha taarifa kutoka kuwa wamefariki.
Habari zaidi zinasema watu hao ambao ni Othman Hamad Othman (75) na Amour Salim Khamis (28) wakazi wa Wete Kaskazini Pemba walijumuishwa na mwenzao Mbarouk Abdalla Khamis anayedaiwa kuwa dhoofu akiandamwa na majeraha ,walikamatwa wakiwa wazima kabla ya taarifa za vifo vyao kutoka.
Mratibu kitaifa wa Mtandao huo Wakili Onesmo Olengurumwa amesema vitendo vya baadhi ya majeshi kujichukulia sheria mkononi kwa kutesa au kuuwa watuhumiwa havikubaliki na kuwa inasikitisha kuona haviheshimu sheria.
“Tuna laani vitendo hivi ambavyo vinafanywa na majeshi haya ambayo yanafanya kazi ambazo kimsingi ,kisheria hawakupaswa kufanya, masuala ya kukamata watu na kufanya uchunguzi,yabaki kuwa ya jeshi la Polisi” amesema Olengurumwa
“ Nchi hii (Bara na visiwani) kumekuwa na changamoto kubwa ya majeshi mengine USU ambayo ni nje ya jeshi la Polisi ,yamepewa mamlaka ya kukamata watu,kufanya uchunguzi,kitu ambacho kwa namna moja au nyingine wamekuwa wakiongeza changamoto nyingine kubwa sana ya utesaji wa watu wanapokuwa wamekamatwa” ameongeza Olengurumwa.
Tayari jeshi la Polisi mkoa wa Kusini Pemba limetoa taarifa ya kuanzisha uchunguzi wa vifo hivyo vya watu waliotuhumiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulvya ambao wanadaiwa kukamatwa usiku wa kuamkia tarehe 24/12/2024, mnamo saa 7 za usiku, wakiwa wazima wa afya .