Рет қаралды 4,196
Gaza. Mamlaka nchini Israel imetoa taarifa kwa Umma kuwa taarifa iliyowasilishwa na kundi la Hamas inaonyesha mateka nane kati ya 33 waliotakiwa kuachiliwa na kundi hilo wameshauawa.
Tovuti ya Al Jazeera, imeripoti kuwa Msemaji wa Serikali ya Israel, David Mencer alivieleza vyombo vya habari jana Jumatatu kuwa mateka 25 wa Israel waliosalia bado wako hai na iko tayari kuwakabidhi wakaungane na familia zao.
Kwa mujibu wa Mencer, taarifa hiyo ilitolewa baada ya kufanyika ufuatiliaji wa hali za mateka walioko mikononi mwa Hamas eneo la Gaza nchini Palestina kujua hali zao za kiafya.
“Tayari tumeshazijulisha familia za mateka waliofariki na tayari mateka nao wameshajulishwa hali za wapendwa wao walioko mikononi mwa Hamas,” alisema Mencer bila kutaja majina ya mateka ambayo wamefariki eneo la Gaza.
Msemaji huyo amesema awamu nyingine ya mabadilishano ya mateka na wafungwa kati ya pande hizo yatafanyika Alhamisi Januari 30,2025, kisha kufuatiwa na mabadilishano yatakayofanyika Jumamosi Februari Mosi, mwaka huu.
Takriban raia 90 wa Israel wanaendelea kushikiliwa mateka eneo la Gaza. Kutokana ma mwenendo huo wa taarifa Serikali nchini Israel inaamini zaidi ya mateka 35 huenda wakawa wameshauawa.
Makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Jeshi la Israel (IDF) na kundi la Hamas yalitangazwa mapema Januari 19 baada ya mazungumzo yaliyodumu kwa muda mrefu yakiratibiwa na taifa la Qatar, Marekani na Misri.
Kufikiwa mwafaka wa kusitisha mapigano hayo, kulitoa fursa ya kukomeshwa vita iliyodumu kwa miezi takriban 15 tangu Hamas ifanye shambulizi la kushtukiza nchini Israel Oktoba 7,2023 kisha IDF kutangaza operesheni maalum ya kukabiliana na kundi hilo.
Katika awamu ya kwanza ya makubaliano hayo, mateka 33 wanaoshikiliwa Gaza wanatarajiwa kuachiwa huru kwenye mabadilishano ya wafungwa zaidi ya 1,900 ambao ni raia wa Palestina wanaotumikia vifungo kwenye magereza ya Israel.
Tayari wanawake saba wa Israel wamenufaika na makubaliano hayo kwa kuachiwa huru huku wafungwa 290 wa Palestina waliokuwa wanatumikia vifungo kwenye magereza ya Israel wakiachiwa.
Katika mabadilishano yatakayofanyika Alhamisi, wanawake watatu raia wa Israel, miongoni mwao ni Arbel Yehud na Agam Berger, wataachiliwa kutoka mikononi mwa Hamas huku mateka mmoja atakayeungana nao akiwa bado jina lake halijaanikwa.
Kuachiliwa kwa mateka hao kulitangazwa na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu juzi (Jumapili) huku akitaja kuwa ni sehemu ya makubaliano hayo.
Kwa mujibu wa Israel, mwanamke mwingginw, Arbel Yehud, alipaswa kuachiliwa Jumamosi iliyopita japo halikuwezekana hadi jana Hamas iliporidhia kumwachia na kumkabidhi kwa maofisa wa taifa hilo.
Kabla ya Yehud kukabidhiwa kwa maofisa wa Israel, taifa hilo liliishutumu Hamas kwa kukiuka matakwa ya makubaliano ya kusitisha vita hiyo huku IDF ikishinikiza aachiwe kwa kuwazuia raia walioyakimbia makazi yao eneo la Gaza kutopita na kurejea kwenye makazi yao. Baada ya kuachiwa mwanamke huyo raia wa Gaza wakaruhusiwa kurejea jana jioni.