Рет қаралды 7,125
Wapiganaji wa kundi la Hamas wamewaachia mateka watatu wa Israel lililokuwa linawashikilia tangu uvamizi uliofanyika Oktoba 7,2023.
Katika makubaliano kati ya pande hizo, Serikali ya Israel imewaachia wafungwa wa kipalestina 183. Wafungwa hao ni waliokuwa wakitumikia vifungo mbalimbali kwenye magereza ya Israel ikiwemo adhabu ya kifo na kifungo cha maisha jela.
Mabadilishano hayo ni ya mara ya tatu tangu pande hizo zikubaliane kusitisha mapigano na kuridhia kuwaachia mateka na wafungwa wa kila pande ambapo hadi sasa mateka 15 wa Israel wamerejeshwa kuungana na familia zao huku wapalestina zaidi ya 350 wakiachiwa huru.
Al Jazeera imeripoti kuwa miongoni mwa mateka wa Israel waliokuwa Gaza walioachiwa leo Jumamosi Februari Mosi,2025, ni Rais wa Israel mwenye asili ya Ufaransa,Ofer Kalderon na raia wa Israeli ambao wote wamekabidhiwa kwa maofisa wa Msalaba Mwekundu mjini Khan Younis.
Baada ya saa moja kupita, Hamas pia imemuachia raia wa Israel mwenye asili ya Marekani, Keith Siegel ambaye amekabidhiwa kwa maofisa wa Msalaba Mwekundu waliokuwa eneo la Kaskazini mwa Gaza nchini humo.
Muda mfupi baada ya raia hao kuwasili nchini Israel, magari yenye wafungwa 183 wa kipalestina wakiwemo watoto waliokuwa kifungoni nchini Israel katika utekelezaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano hayo yaliyofikiwa Januari 19,2025, Doha nchini Qatar.
Wafungwa 73 kati ya 183 wa Palestina walikuwa wakitumikia adhabu ya kifungo cha maisha katika magereza mbalimbali nchini Israel.
Tayari basi la kwanza lililobeba wapalestina 32 kutoka gereza la Ofer nchini Israel limewasili mjini Ramallah ukanda wa Magharibi mwa Gaza, huku wakipolekewa na mamia ya raia waliokuwa wanawasubiria eneo hilo.
Miongoni mwa walioachiwa ni wazee wa Kipalestina waliokuwa kifungoni kwa muda mrefu nchini Israel kutokana na mzozo wa pande hizo ambao umedumu kwa karibia nusu Karne, wengine walikuwa kwenye viti vya kusukuma (Wheelchair).
Mbali na hao, wapalestina 111 kati ya 183 walioachiwa leo walichukuliwa na majeshi ya Israel baada ya shambulizi la Oktoba7, 2023. Baada ya kuachiwa, saba kati yao watapelekwa uhamishoni nchini Misri.
Inakadiriwa kuwa kuna wapalestina takriban 4,500 katika magereza ya Israel wakitumikia vifungo mbalimbali wakishikiliwa katika kile kinachoitwa ni vifungo vya kiutawala ambavyo vinawazuia kushtakiwa badala yake kuamriwa kutumia kifungo jela bila kushtakiwa.
Mapema leo asubuhi wapiganaji wa Hamas wameonekana wakipanga mistari huku wakiwatuliza umati wa raia wa Palestina waliojitokeza kushuhudia kuachiwa kwa mateka hao eneo la Mji wa Gaza na Khan Younis. Baada ya kufikishwa, mateka hao, Kalderon, Bibas na Siegel waliwapungia mikono umati huo.
Mateka wote wameshafika nchini Tel Aviv nchini Israel ambako watafanyiwa uchunguzi wa kitabibu kubaini hali ya afya zao kabla ya kuungana na familia zao.
Hadi sasa hali za kiafya za mke wa Bibas na watoto wawili waliochukuliwa mateka na Hamas bado hazijulikani zikoje.
Luciano Zaccara, ambaye ni Profesa wa Chuo Kikuu cha Qatar aaliyebobea katika mzozo ya Mashariki ya Kati anasema kuachiwa kwa mateka hao ni ishara kwamba Hamas bado ina nguvu ya kuendelea kulisimamia eneo la Gaza pamoja na mashambulizi mfululizo ya IDF yaliyofanyika eneo hilo kwa miezi zaidi ya 15.
“Pamoja na kuwa Israel ilidai kuwasambaratisha Hamas lakini picha hazidanganyi kwamba Hamas bado wapo na bado wanamsukumo kwa Umma,”
“Mabadilishano haya yanafanyika bila kikwazo chochote kiasi kwamba yanatoa picha kwamba huenda mabadilishano yanayofuata huenda yasiwe na changamoto yoyote,” amesema Profesa Zaccara.
Mchambuzi wa Siasa za Mashariki ya Kati kutoka Chuo Kikuu cha Burzeit, Basil Farraj amesema kuachiwa kwa wafungwa wa palestina hakuondoi maumivu ya wapalestina na Hamas ambayo yameyapitia kwenye mashambulizi mfululizo ya Israel katika ardhi yao.
Ametahadharisha kuwa baada ya mabadilishano hayo huenda Israel ikarejea tena kuwakamata raia hao wa Palestina na kuibua tena mzozo kati ya pande hizo.
Kulingana na makubaliano hayo, siku ya Jumanne huenda mateka zaidi ya 60 wa Israel wakaachiwa huku wafungwa wa Palestina wengi zaidi wakaachiwa kutoka katika magereza ya Israel.
Makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya pande hizo yaliratibiwa na mataifa ya Qatar, Marekani na Misri.
Wakati mabadilishano hayo yakifanyika, Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema wapalestina takriban 50 wako kwenye uhitaji wa hali ya juu wa kupatiwa matibabu nje ya nchi hiyo na wanatarajiwa kuvushwa kupitia mpaka wa Rafah kuhudhuria matibabu hayo.
Pia Jeshi la Israel (IDF) linashutumiwa kutekeleza shambulizi kwa kutumia boti iliyokuwa ikipita baharini na kurusha risasi karibia na Kambi ya Wakimbizi ya Nuseirat Gaza nchini humo na kusababisha kifo cha mvuvi katika eneo hilo.