Рет қаралды 28,699
Familia katika Mji wa Goma Mashariki mwa Jamhuri y Kidemokrasia ya Congo (DRC) zimeanza kuendesha maziko ya wapendwa wao waliofariki kwenye mapigano kati ya wapiganaji wa kundi la M23 dhidi ya vikosi vya Jeshi la Ulinzi la nchi hiyo (FARDC).
Tovuti ya Al Jazeera imeripoti kuwa hadi kufikia jana takriban miili 2,000 ya watu waliouawa katika mapigano hayo ilikuwa imehifadhiwa katika vituo vinavyosimamiwa na Msalaba Mwekundu katika Mji wa Goma nchini humo.
Hata hivyo, Umoja wa Mataifa katika taarifa yake ya juzi, ulisema zaidi ya watu 900 wakiwemo raia wasio na hatia walithibitika kuuawa katika mapigano hayo jambo ambalo limesababisha maafa nchini humo.
Kwa mujibu wa Waziri wa Mawasiliano nchini DRC, Patrick Muyaya, kutokana na uwezekano wa kuwepo hatari ya magonjwa ya mlipuko katika mji wa Goma, mamlaka kwa kushirikiana na Msalaba Mwekundu, na familia zimeanza jana (Jumanne) kufanya maziko ya pamoja ya miili hiyo.
Muyaya amesema baadhi ya miili imeshatambuliwa na ndugu zao huku mingine iliyoshindikana kubainika ikizikwa katika makaburi ya pamoja katika mji huo. Pia amesema athari za mapigano hayo huenda zikaongezeka.
Julienne Zaina Barabara, ambaye ni Mkazi wa Katoyi Mjini Goma, alisema mtoto wake wa kike aliuawa wiki iliyoisha katika mapigano hayo huku wawili wakijeruhiwa baada ya bomu kurushwa karibu na makazi yao.
“Tuliwachukua tukawapeleka hospitalini hata hivyo mmoja wao alifariki baada ya saa moja kupita. Wawili bado wanaendelea na hospitalini, baada ya kufanyiwa uchunguzi mmoja wao amebainika na jeraha kubwa kichwani,” amesema Julienne.
Kutokana na kukatika kwa umeme katika Mji wa Goma, majengo ya kuhifadhia maiti (mochwari) zimekosa uwezo wa kuendelea kuhifadhi miili hiyo jambo lililozilazimu mamlaka kuchukua hatua ya kuizika haraka iwezekanavyo kabla haijarabika.
Mkuu wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu Kusini mwa Goma, Myriam Favier, amesema kwa sasa wanakimbizana na muda ili kutoruhusu miili hiyo kuharibika kabla ya kuzikwa na kusababisha mlipuko wa magonjwa katika eneo hilo.
Jana Muungano wa Makundi ya waasi nchini DRC, likiiwemo kundi la M23, ulitoa taarifa ya kusitisha mapigano dhidi ya vikosi vya Serikali kwa kile ambacho ulidai ni Janga la kibinadamu lililoibuka nchini humo.
Taarifa Alliance Fleuve Congo ya kundi la M23 (AFC/M23), iliyotolewa jana Jumatatu Februari 3, 2025, kwa Umma ilisema:
“Muungano wa Alliance Fleuve Congo (AFC/M23), unautangazia umma kuwa kwa kuzingatia janga la kibinadamu lililosababishwa na utawala wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), tumesitisha mapigano kuanzia leo Februari 4, 2025, kwa sababu za kibinadamu.”
Taarifa hiyo imeenda mbali na kulishutumu Jeshi la Ulinzi la DRC la FARDC, kwa kutumia ndege za kijeshi kutekeleza mashambulizi yaliyosababisha mauaji ya wapiganaji wake karibia na uwanja wa ndege wa Kavumu nchini humo.
“Ifahamike kuwa hatuna lengo la kuuteka Mji wa Bukavu ama maeneo mengine, bali tunalenga kupigania na kulinda maslahi ya raia wa DRC,” imesema taarifa.
Umesema: “Tunaitaka SAMIDRC (Jeshi la Umoja wa Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika), kuondoa vikosi vyake nchini DRC, kwa sababu lengo ambalo lilisababisha walinda amani hao kuwepo nchini DRC limeshatoweka.”
Waasi wa kundi la M23, walianza operesheni yao ya kuitwaa miji ya Mashariki wa DRC hususan Mji wa Goma uliopo katika Jimbo la Kivu Kaskazini mwishoni mwa mwezi Januari 2025, kisha kutangaza kujitanua na kuahidi kufanya maandamano hadi Mji Mkuu wa Taifa hilo wa Kinshasa.
Imeandikwa kwa msaada wa Mashirika.