Рет қаралды 4,328
Washington. Televisheni ya CBS news imeripoti kuwa tayari miili ya watu 18 imeshanasuliwa kutoka kwenye maji ya mto ambao ajali ya ndege ya abiria ya Shirika la Marekani iliyogongana na Helkopta ya Jeshi la nchi hiyo aina ya UH-60 ‘Black Hawk’.
Ajali hiyo imetokea usiku wa kuamkia leo Alhamisi Januari 30,2025 katika uwanja wa ndege wa kitaifa wa Reagan wakati ndege hiyo ikienda kutua katika uwanja wa ndege wa kitaifa wa Reagan jijini Washington DC.
Ndege hiyo ya abiria ya Shirika la ‘American Airlines’ namba 5342 ilikuwa na abiria 60 na wahudumu wanne huku Helkopta ya kijeshi ikiwa na wanajeshi watatu waliokuwa kwenye mafunzo.
Kwa mujibu wa CBS news, tayari maofisa wa dharura na uokozi zaidi ya 300 wamewasili ulipo Mto Potomac uliopo karibu na Ikulu ya Washington nchini humo ambapo ndipo ndege hizo zimeanguka baada ya kugongana.
Vyombo vingine vya habari ikiwemo the Washington Post, vimeripoti kuwa hadi sasa hakuna manusura aliyepatika katika jitihada za uokoaji zinazofanywa na maofisa zaidi ya 300 walioko eneo hilo. Hata hivyo imedai kushuhudia miili ya watu ikitolewa majini.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la ndege la Marekani, Robert Isom ametoa taarifa kwa Umma akisema: “Sasa hivi tumejikita kuangalia usalama wa abiria waliokuwemo, wahudumu na familia zao, tunaendelea kuwasiliana na mamlaka husika kuhusiana na suala hili sambamba na kutoa huduma za dharura,”
Kufuatia ajali hiyo, Rais Donald Trump ameeleza kukasirishwa nayo huku akisema ajali hiyo ingeweza kuepukika huku akiwanyooshea kidole wasimamizi wa uwanja wa ndege ilipotakiwa kutua ndege hiyo.
“Ajali hii ingeweza kuzuilika. Kwa nini wafanyakazi waliokuwa kwenye mnara wa kuongozea ndege wasingewaambia wanajeshi waliokuwa ndani ya Helkopta mbinu mbadala ya kufanya baada ya kuona ndege hiyo ikielekea kutua. Mazingira ya ajali hiii yanaonekana wazi kuwa ingeweza kuzuilika,” amesisitiza Trump.
Trump ameandika ujumbe huo kwenye akaunti ya mtandao wake wa Truth Social huku akisisitiza kuwa hajafurahishwa hata kidogo na mazingira ya ajali hiyo.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.